Askari wa Uganda waua magaidi 22 wa Al-Shabaab nchini Somalia
(last modified Mon, 02 Apr 2018 07:39:59 GMT )
Apr 02, 2018 07:39 UTC
  • Askari wa Uganda waua magaidi 22 wa Al-Shabaab nchini Somalia

Jeshi la Uganda UPDF limesema askari wake walio katika Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika Somalia, AMISOM, wamewaua magaidi 22 wa kundi la al-Shabab.

Katika taarifa aliyoitoa, naibu msemaji wa jeshi la UPDF Kalani Deo Akiiki, amesema askari hao wa UPDF wamewaua magaidi hao wakati walipojaribu kushambulia kambi zilizoko Quoroyole, Buulo Mareer na Golwen katika mkoa wa Lower Shabelle nchini Somalia.

Taarifa pia imesema, askari wanne wa jeshi la UPDF wameuawa na wengine sita kujeruhiwa katika mapambano hayo yaliyoibuka jana  Jumapili asubuhi. Aidha, magari manane ya magaidi hayo yakiwemo mawili yaliyotegwa mabomu yameteketezwa, na kukamatwa silaha za aina tofauti.

Hayo yanajiri wakati ambao hivi karibuni mkuu wa AMISOM alitahadharisha kuwa huenda ndoto ya kuwaondoa maelfu ya askari wake katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika isitimie bila msaada wa dharura na uungaji mkono wa jamii ya kimataifa.

Francisco Madeira, Mkuu wa AMISOM alisema kuna wasi wasi mkubwa kwamba huenda mafanikio yote waliyoyapata katika kipindi cha muongo mmoja uliopita yakaporomoka, iwapo wataondoa ghafla askari wote 21 elfu wa kikosi hicho bila kuweka mikakati madhubuti ya kukabidhi mikoba kwa maafisa usalama wa Somalia.

Kikosi cha Amisom ambacho kiliundwa kupitia azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kimekuwa kikiisaidia serikali ya Somalia kupambana na magaidi wa kundi la al Shabab tangu mwaka 2007.  Kikosi hicho kinaundwa na askari kutoka nchi za Uganda, Kenya, Djibouti, Burundi na Ethiopia.

Tags