Hali ya Burundi yatiliwa wasiwasi na Baraza la Usalama la UN
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeeleza wasiwasi wake kuhusiana na hali ya kisiasa nchini Burundi sambamba na ukosefu wa irada thabiti ya kisiasa ya kuupatia ufumbuzi mgogoro uliopo.
Taarifa ya rais wa baraza hilo imezitaka pande husika za kisiasa nchini humo kushiriki pasina na masharti yoyote kwenye mazungumzo ya amani yanayoongozwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC.
Hivi karibuni, Michel Kafando, Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi aliliambia Baraza la Usalama la umoja huo kwamba mgogoro wa nchi hiyo unatia wasiwasi, na kwamba Umoja wa Afrika unapaswa kuimarisha juhudi za upatanishi nchini humo.
Mwezi uliopita, Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi alitangaza Mei 17 kuwa tarehe ya kufanyika kura ya maoni ya kuifanyia mabadiliko katiba ya nchi, na iwapo kwa uchache asilimia 50 ya wapiga kura wataunga mkono mabadiliko hayo ya katiba, watakuwa wamemsafishia njia Nkurunziza ambaye amekuwa madarakani tokea mwaka 2005, kusalia uongozini hadi mwaka 2034.
Burundi ilitumbukia katika machafuko ya ndani mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka 2015 baada ya chama tawala cha CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza kugombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita kwa mara ya tatu mfululizo kinyume na makubaliano ya Arusha.
Tangu wakati huo mamia ya watu wameuawa na maelfu wamelazimika kukimbilia katika nchi jirani kutokana na ghasia na machafuko ya ndani.