Wahajiri 11 wa Kiafrika wamekufa maji katika pwani ya Libya
Kwa akali wahajiri 11 wa Kiafrika wameripotiwa kufariki dunia baada ya boti yao kuzama katika maji ya pwani ya magharibi mwa Libya, wakati wakiwa safarini kuelekea Ulaya.
Jenerali Ayoub Kacem, Msemaji wa Jeshi la Majini la Libya amesema miili ya wahajiri hao waliokuwa na nia ya kwenda kutafuta hifadhi barani Ulaya ilipatikana ikielea nje ya mji wa Sabratha, karibu na mji wa Zliten, katika operesheni mbili za uokoaji zilizofanywa na Gadi ya Pwani ya Libya hapo jana.
Afisa huyo wa Jeshi la Baharini la Libya ameongeza kuwa, wahajiri wengine 263 wameokolewa katika operesheni hiyo.
Februari mwaka huu, Shirika la Kimataifa la Wahajiri (IOM) lilitangaza kuwa, wahajiri haramu wapatao 90 wameaga dunia katika maji ya pwani ya Libya baada ya boti yao kuzama baharini.
Kwa mujibu wa IOM, zaidi ya wakimbizi elfu tatu waliaga dunia mwaka jana wakijaribu kufika Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania, akthari ya wahajiri hao wakiwa ni raia wa nchi za Kiafrika ambao wanataraji kupata maisha mazuri na ajira huko barani Ulaya.
Zaidi ya watu 87,000 walihatarisha maisha yao katika safari hizo za baharini za kuogofya, wakijaribu kufika Yemen mwaka jana pekee.