SADC yajadili mgogoro wa kisiasa unaoshuhudiwa Kongo DR
Viongozi wa Jumuiya ya Ustawi ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC wameanza kujadili mgogoro wa kisiasa unaoshuhudiwa hivi sasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa SADC walikutana jana Jumapili katika mji mkuu wa Angola, Luanda katika mkutano ambao kilele chake ni kikao cha marais na viongozi wa serikali wa nchi wanachama hapo kesho Jumanne.
Marais wa nchi wanachama zikiwemo Namibia, Afrika Kusini, Zambia, Swaziland (eSwatini), DRC na Lesotho wamethibitisha kuwa watashiriki kikao hicho, huku Tanzania ikitazamiwa kuwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa tangu Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo akatae kung'atuka madarakani baada ya kumalizika muhula wake wa uongozi mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka 2016 na kuendelea kuahirishwa uchaguzi kwa mara kadhaa.
Mwezi uliopita, Umoja wa Mataifa ulilaani hatua ya askari usalama wa Kongo DR ya kuwaua raia wa nchi hiyo karibu 50 wakiwemo wanawake na watoto katika kamatakamata na hatua za mabavu zilizo kinyume cha sheria, zilizochukuliwa na askari hao dhidi ya wafanya maandamano mwaka jana na mwanzoni mwa mwaka huu.
Kadhalika SADC inajadili mgogoro wa kisiasa unaoendelea kutokota nchini Lesotho. Katika kipindi cha hivi karibuni, Lesotho imekuwa ikishuhudia mgogoro wa madaraka na uingiliaji wa jeshi katika masuala ya kisiasa nchini humo.