Misri na Imarati zatuhumiwa kuvuruga mchakato wa mapatano ya kitaifa Libya
Jumuiya ya International Action Group for Libya imezituhumu nchi za Imarati na Misri kuwa zinavuruga jitihada zinazofanywa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mapatano ya kitaifa nchini Libya.
Taarifa iliyotolewa na International Action Group for Libya imeikosoa Imarati kwa kukwamisha juhudi zinazofanywa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya na kutangaza kwamba, hatua hiyo si ya kibinadamu. Jumuiya hiyo pia imeituhumu Imarati kuwa inawapatia rushwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa nchini Libya kwa shabaha ya kupendelea upande mmoja katika mzozo wa kisiasa wa nchi hiyo na kwa ajili ya kuzusha machafuko na ghasia.
Taarifa ya International Action Group for Libya imesisitiza kuwa, Imarati ilimpa rushwa mjumbe wa zamani wa Umoja wa Mataifa huko Libya, Bernardino Leon ili azushe hitilafu na mivutano kati ya makundi mbalimbali ya nchi hiyo.
Taarifa hiyo pia imesema kuwa, mjumbe wa sasa wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya, Ghassan Salamé amenyamazia kimya mauaji yanayofanywa na makundi ya wanamgambo katika miji kama Benghazi na Sabha na kwamba hajachukua hatua yoyote ya kukomesha mzingiro dhidi ya watu wa mji wa Derna ulioko kaskazini mashariki mwa Libya.