UN yagundua makaburi matano ya umati mkoani Ituri Kongo DR
Umoja wa Mataifa umetangaza habari ya kugundua makaburi mengine matano ya umati katika mkoa wa Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Taarifa ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa huko DRC imesema kuwa, makaburi hayo ya umati yamegunduliwa katika maeneo ya mpaka wa nchi hiyo na Uganda, Rwanda na Burundi yaliyoshuhudia mapigano kati ya wakulima wa kuhamahama wa kabila la Lendu na wafugaji wa kabila la Hema, ambapo watu zaidi ya 260 waliuawa.
Hata hivyo timu ya uchunguzi ya UN haijatoa maelezo zaidi kuhusu makaburi hayo ya umati na idadi ya miili iliyopatikana, lakini imesema miji na vijiji 120 vilishuhudiwa umwagikaji mkubwa wa damu katika mapigano hayo yaliyofanyika kati ya Disemba mwaka jana na katikati ya mwezi uliopita wa Machi.
Mashambulizi ya wakulima wa kuhamahama wa kabila la Lendu yamesababisha watu zaidi ya 60 elfu wakimbilie usalama wao katika nchi jirani ya Uganda kupitia Ziwa Albert.
Kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, Wakongamani zaidi ya laki mbili wanatazamiwa kuingia Uganda wakitoroka mapigano hayo kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Mwezi Julai mwaka jana, Ofisi ya Askari wa Kulinda Amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilitangaza kuwa imegundua makaburi mengine ya umati yapatayo 38 katika maeneo sita tofauti katika operesheni ya pamoja na maafisa wa uchunguzi wa jeshi la DRC katika eneo la magharibi mwa Kasai.