Watu 40 wazama mtoni DRC wakitoroka mapigano
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i43732-watu_40_wazama_mtoni_drc_wakitoroka_mapigano
Raia wapatao 40 wamezama mtoni baada ya boti zao kukumbwa na dhoruba na kuzama wakati wa kuvuka mto uliokuwa umefurika wakati wakitoroka mapigano kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 27, 2018 23:26 UTC
  • Watu 40 wazama mtoni DRC wakitoroka mapigano

Raia wapatao 40 wamezama mtoni baada ya boti zao kukumbwa na dhoruba na kuzama wakati wa kuvuka mto uliokuwa umefurika wakati wakitoroka mapigano kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Akizungumza Ijumaa, Naibu Gavana wa Ubangi Kusini Jean Bakatoye amesema hadi sasa ni miili 40 iliyooplewa kufuatia tukio hilo la Jumatano.

Amesema idadi ya waliofariki inatazamiwa kuongezeka kwani miili zaidi inaweza kupatikana katika maeneo unakopitia mto huo.

Raia hao walikuwa wanajaribu kuvuka Mto Ubangi ambao ni sehemu ya mpaka wa nchi hiyo na Jamhuri ya Kongo. Bakatoye amesema raia hao walikuwa wakitoroka mapigano baina ya wanajeshi wa DRC na watu aliowataja kuwa wahalifu.

Mapigano hayo yalijiri katika eneo la mpakani la Dongo baada ya wanajeshi kuvamiwa na watu waliokuwa na silaha.

Rais Joseph Kabila

Eneo la Dongo lilikumbwa na uasi wa kabila la Enyele mwaka 2009, uasi ambao ulizimwa na Jeshi la DRC. Karibu watu 270 waliuawa katika mapigano hayo na wengine zaidi ya laki mbili kulazimika kuyakimbia makazi yao.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa tangu Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo akatae kung'atuka madarakani baada ya kumalizika muhula wake wa uongozi mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka 2016 na kuendelea kuahirishwa uchaguzi mara kadhaa.