Maandamano dhidi ya rais wa Madagascar yanaendelea
Zaidi ya wanaharakati 1,000 wanaoipinga serikali ya Madagascar wameendelea na maandamano yao kwa siku ya nane mfululizo wakimtaka rais wa nchi hiyo ajiuzulu.
Leo waandamanaji hao wamekusanyika katika uwanja mmoja mbele ya ukumbi maarufu mjini Antananarivo wakishinikiza kujiuzulu Rais Hery Rajaonarimampianina.
Moja ya mabango yaliyokuwa yemebebwa na wanaharakati hao lilikuwa na maneno yasemayo: "Toka, Rajao, muuaji na katili wa kutisha."
Mwanasheria wa kambi ya upinzani, Lanto Rakotomanga amewaambia waandamanaji hao kwamba lazima sasa tusitumie tena neno 'rais' kwa sababu Rajao zi rais wetu tena.
Wapinzani hao wamesema, serikali inafanya njama za kuwatoa katika kinyang'anyiro cha kuwania kiti cha urais na katika uchaguzi wa bunge uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Novemba au mwezi Disemba mwaka huu kwa mujibu wa sheria mpya za uchaguzi.
Wapinzani hao wa serikali ya Madagascar wanasema kuwa sheria hizo zimewekwa ili kumbeba Rajaonarimampianina na kuwazuia wanasiasa wa upinzani kushiriki katika uchaguzi.
Wabunge wa upinzani wameitaka mahakama ya katiba ya nchi hiyo kumfuta kazi rais huyo.
Wiki iliyopita watu wawili waliuawa na wengine 16 walijeruhiwa katika siku ya kwanza ya maandamano hayo ya kupinga serikali huku rais wa Madagascar akidai kuwa wapinzani wanataka kumpindua kinyume cha sheria.