Mwendesha Mashtaka wa ICC yuko DRC kuchunguza jinai dhidi ya binadamu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i43956-mwendesha_mashtaka_wa_icc_yuko_drc_kuchunguza_jinai_dhidi_ya_binadamu
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, yuko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuchunguza jinai za kutisha zilizofanyika na zinazoendelea kufanyika nchini humo.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
May 02, 2018 10:25 UTC
  • Mwendesha Mashtaka wa ICC yuko DRC kuchunguza jinai dhidi ya binadamu

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, yuko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuchunguza jinai za kutisha zilizofanyika na zinazoendelea kufanyika nchini humo.

Fatou Bensouda aliwasili mjini Kinshasa jana Jumanne, ambapo anatazamiwa kukutana na viongozi wa serikali na mhimili wa mahakama kabla ya kufanya kikao na waandishi wa habari kesho Alkhamisi.

Machi Mosi, harakati ya kijamii ya Debout nchini Kongo iliiandikia barua ICC, ikiitaka ichunguze jinai zinazofanyika nchini humo, na haswa kushambuliwa kwa waandamana na vyombo vya usalama. Aidha Januari mwaka huu, Bunge la Umoja wa Ulaya lilipasisha azimio likiutaka Umoja wa Mataifa na ICC kuchunguza jinai zilizoigubika nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa madini ya katikati mwa Afrika.

Makumi ya watu wameuawa tangu Disemba 31 mwaka jana hadi sasa baada ya kukabiliwa na maafisa usalama wa DRC, kwa kushiriki maandamano yaliyoitishwa na viongozi wa Kanisa Katoliki nchini humo kupinga uongozi wa Rais Joseph Kabila.

Maafisa wa polisi DRC wakikabiliana na waandamanaji

Mwaka jana ICC ilitahadharisha kuwa ukatili uliofanyika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikiwa ni pamoja na mauaji ya wataalamu wawili wa Umoja wa Mataifa unaweza kutambuliwa kuwa ni jinai ya kivita.

Hii ni katika hali ambayo, viongozi wengi wa nchi za Afrika wamekuwa wakikosoa vikali utendaji wa ICC, ambapo mwishoni mwa mwezi uliopita, Rais Paul Kagame wa Rwanda alisema kuwa mahakama hiyo yenye makao yako mjini The Hague nchini Uholanzi imefeli katika kutekeleza uadilifu, kwa kuwaandamana tu viongozi wa Afrika.