Kanisa Katoliki nchini Burundi lapinga kura ya maoni
Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Burundi wamepinga kura ya maoni ya kuifanyia marekebisho katiba ya nchi inayotazamiwa kufanyika mwezi huu.
Taarifa iliyosainiwa na maaskofu 10 wa ngazi za juu wa kanisa hilo imesema kuwa, huu sio wakati mwafaka wa kuifanyia marekebisho katiba kutokana na hali mbaya ya kisiasa na kiusalama inayoshuhudiwa nchini humo.
Huku ikivilaumu vyombo vya usalama kwa kueneza taharuki na vitisho kwa wapinzani na wakosoaji wa serikali, taarifa hiyo imeongeza kuwa, "Raia wengi ingawaje hawalisemi hili hadharani, lakini wanaishi kwa woga kiasi cha kutozungumzia maoni yao ya kweli wazi wazi, wakihofia kuandamwa na vyombo vya dola."
Kadhalika vyama vingi vya upinzani vimeonesha kutokubaliana na marekebisho hayo ya katiba, baadhi vikitangaza kuwa vitasusia kura hiyo ya maoni, na vingine vikiwataka wafuasi wao kuyapigia marekebisho hayo ya katiba kura ya la.
Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi alitangaza Mei 17 kuwa tarehe ya kufanyika kura ya maoni ya kuifanyia mabadiliko katiba ya nchi, na iwapo kwa uchache asilimia 50 ya wapiga kura wataunga mkono mabadiliko hayo ya katiba, watakuwa wamemsafishia njia Nkurunziza ambaye amekuwa madarakani tokea mwaka 2005, kusalia uongozini hadi mwaka 2034.
Burundi ilitumbukia katika machafuko ya ndani mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka 2015 baada ya chama tawala cha CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza kugombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita kwa mara ya tatu mfululizo kinyume na makubaliano ya Arusha.
Tangu wakati huo mamia ya watu wameuawa na maelfu wamelazimika kukimbilia katika nchi jirani kutokana na ghasia na machafuko ya ndani.