Taharuki Burundi, maafisa wa serikali wataka 'kuhasiwa maadui'
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i44220-taharuki_burundi_maafisa_wa_serikali_wataka_'kuhasiwa_maadui'
Huku zikiwa zimesalia chini ya wiki mbili kabla ya wananchi wa Burundi kushiriki kwenye kura ya maoni ya kuifanyia marekebisho katiba ya nchi, hali ya taharuki imetanda nchini humo huku maafisa wa serikali wakitoa mwito wa kushambuliwa watu wanaopinga kufanyika kwa zoezi hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 08, 2018 12:31 UTC
  • Taharuki Burundi, maafisa wa serikali wataka 'kuhasiwa maadui'

Huku zikiwa zimesalia chini ya wiki mbili kabla ya wananchi wa Burundi kushiriki kwenye kura ya maoni ya kuifanyia marekebisho katiba ya nchi, hali ya taharuki imetanda nchini humo huku maafisa wa serikali wakitoa mwito wa kushambuliwa watu wanaopinga kufanyika kwa zoezi hilo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press, baadhi ya maafisa wa serikali wamesikika hadharani wakitoa mwito wa 'kuhasiwa maadui'.

Shirika hilo la habari limenukuu mashirika ya kutetea haki za binadamu yakisema kuwa, idadi kubwa ya watu wanaaonekana kuwa wapinzani wa serikali na zoezi hilo la kura ya maoni ama wameuawa au kukamatwa na vyombo vya usalama.

Kanisa Katoliki na vyama vingi vya upinzani nchini humo vimeonesha kutokubaliana na marekebisho hayo ya katiba, baadhi vikitangaza kuwa vitasusia kura hiyo ya maoni, na vingine vikiwataka wafuasi wao kuyapigia marekebisho hayo ya katiba kura ya la. 

Rais Nkurunziza wakati wa kuanza kampeni za kuunga mkono kura ya maoni

Siku chache zilizopita serikali ya Burundi ilitangaza kuyapiga marufuku mashirika ya utangazaji ya BBC ya Uingereza na VOA ya Marekani kutokana na kile ilichotaja kama kukiuka maadili na sheria za vyombo vya habari.

Burundi ilitangaza Mei 17 kuwa tarehe ya kufanyika kura ya maoni ya kuifanyia mabadiliko katiba ya nchi, na iwapo kwa uchache asilimia 50 ya wapiga kura wataunga mkono mabadiliko hayo ya katiba, watakuwa wamemsafishia njia Rais Pierre Nkurunziza ambaye amekuwako madarakani tokea mwaka 2005, kusalia uongozini hadi mwaka 2034.