ICC yataka msaada wa Baraza la Usalama kumkamata Seiful Islam Gaddafi
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imeliomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuisaidia katika kuwakamata watu watatu wanaosakwa nchini Libya akiwemo Seiful Islam, mwana wa kiume wa aliyekuwa kiongozi wa wa nchi hiyo, Kanali Muammar Gaddafi.
Fatou Bensouda, Mwendesha Mashitaka Mkuu wa ICC ameliambia baraza hilo kuwa, kuna haja ya kukamatwa Seiful Islam Gaddafi pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Usalama Libya, Al-Tuhamy Mohamed Khaled, na Busayf Al-Werfalli, Kamanda wa Brigedi ya Al-Saiqa inayotuhumiwa kuua raia 33; ili wakajibu tuhuma zinazowaandama za jinai za kivita na mauaji.
Bensouda amesema hana habari kuhusu aliko Seiful Islam tangu iripotiwe kwamba amepata msamaha na kuachiliwa huru mnamo Juni 2014, na hajui iwapo bado anazuiliwa au la.
Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC amebainisha kuwa, kukamatwa watatu hao na kukabidhiwa kwa mahakama hiyo iliyoko mjini The Hague nchini Uholanzi ni muhimu sana wakati huu kuliko wakati mwingine wowote.
Mwezi Machi mwaka huu, Aiman Bouras, Mkuu wa Mipango wa SeifuI slam Gaddafi alifichua kuwa mwana huyo wa kiongozi wa zamani wa Libya Kanali Muammar Gaddafi ameandikisha jina lake la kuwa miongoni mwa wagombea katika uchaguzi ujao wa rais nchini humo.
Alisisitiza kuwa Seiful Islam yuko huru licha ya Jenerali Khalifa Haftar kusema kuwa, mwana huyo wa kiume wa Gaddafi angali anashikiliwa katika moja ya jela za Libya.