Makumi ya maelfu wahajiri haramu wa Ghana wakwama nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i44756-makumi_ya_maelfu_wahajiri_haramu_wa_ghana_wakwama_nchini_libya
Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya wakimbizi nchini Libya amesema kuwa, kuna makumi ya maelfu ya wahajiri haramu wa Ghana waliokwama nchini Libya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 20, 2018 10:09 UTC
  • Makumi ya maelfu wahajiri haramu wa Ghana wakwama nchini Libya

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya wakimbizi nchini Libya amesema kuwa, kuna makumi ya maelfu ya wahajiri haramu wa Ghana waliokwama nchini Libya.

Sylvia Lopez-Ekra amesema hayo na kuongeza kuwa, zaidi ya wakimbizi haramu 62 elfu raia wa Ghana bado wamekwama katika hali mbaya nchini Libya na hawana uwezo wa kurejea nchini kwao.

Mkuu huyo wa ofisi ya Umoja wa Mataifa katika masuala ya wakimbizi nchini Libya ameongeza kuwa, juhudi za mashirika ya misaada ya kimataifa za kuwarejesha kwao wakimbizi hao zingali zinaendelea.

Wakimbizi haramu raia wa Ghana katika foleni ya kurejeshwa nyumbani kutoka Libya

 

Inasemekana kuwa nchi zenye wakimbizi wengi haramu huko Libya ya kwanza ni Niger yenye zaidi ya wakimbizi 78,723, ya pili ni Misri yenye wakimbizi 78,616 na ya tatu ni Ghana ambayo hivi sasa ina wakimbizi haramu 62,000 walioorodheshwa na Umoja wa Mataifa huko Libya.

Libya ndiyo njia kubwa ya wakimbizi wa Kiafrika wanaohatarisha maisha yao katika safari hatari mno za kuelekea barani Ulaya kwa tamaa ya kuwa na maisha mazuri.

Magenge ya biashara haramu za magendo ya wanadamu yanatumia fursa ya kukosekana usalama na serikali kuu yenye nguvu huko Libya kuingiza makumi ya maelfu ya wakimbizi nchini humo kila mwaka yakiwarubuni kuwa yatawafikisha barani Ulaya. Asilimia kubwa ya wakimbizi hao hawafiki wanakokwenda bali imma kuzama baharini au hupigwa mnada kama bidhaa masokoni au huishia kwenye makucha ya magenge ya watu hatari.