Watu wanne wauawa, kujeruhiwa katika shambulizi la kigaidi nchini Libya
Kwa akali watu wawili wameuawa na wengine wawili kujeruhiwa kufuatia shambulizi la bomu lililotekelezwa na kundi moja la kigaidi katika mji wa Ajdabia, mashariki mwa Libya.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, hujuma hiyo ya jana Jumanne ilitokea kusini magharibi mwa mji huo, ambapo askari wawili wa jeshi la Libya waliuawa na wengine wawili kujeruhiwa.
Machi 30 mwaka huu, kundi hilo la kigaidi lilifanya shambulizi jingine lililoua watu sita na kuwajeruhi wengine kadhaa.
Libya ilitumbukia kwenye machafuko tangu mwaka 2011 wakati wa kampeni za kuung'oa madarakani utawala wa Kanali Muammar Gaddafi.
Marekani na nchi za Magharibi ziliivamia kijeshi nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, zikafanya uharibifu wa kupindukia kwenye miundombinu ya nchi hiyo na baadaye kuitelekeza huku silaha zikiwa zimezagaa mikononi mwa makundi hasimu.
Tangu wakati huo hadi leo Libya haijawahi kushuhudia utulivu hata siku moja kutokana na kila kundi kuendelea kupigania madaraka na nafasi kubwa zaidi nchini humo.