May 23, 2018 07:37 UTC
  • War Child: Watoto wanajiunga na makundi ya waasi 'kwa khiari' DRC

Shirika la kimataifa la kutetea haki za watoto walioathiriwa na migogoro duniani la War Child limesema aghalabu ya watoto wadogo wanaoujiunga na makundi ya waasi wanaobeba silaha katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanafanya hivyo kwa khiari kwa sababu hawana chaguo mbadala.

Utafiti wa shirika hilo umebainisha kuwa, umaskini, ukosefu wa ajira, njaa na ghasia ni miongoni mwa mambo yanayowasukuma watoto hao kujiunga na magenge hayo ya waasi kwa khiari haswa katika mikoa ya Kivu Kusini na Kivu Kaskazini.

Ripoti ya utafiti huo wa shirika la War Child imefafanua kuwa, kusajiliwa watoto kujiunga na magenge hayo pasina kulazimishwa kumetokana na ukosefu wa machaguo mengine ya kijamii na kiuchumi kwa watoto hao. 

Wapiganaji wa mwituni wakiwasajili watoto DRC

Maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamekuwa yakishuhudia wimbi la machafuko kutokana na uepo wa makundi ya wabeba silaha ambayo pamoja na mambo mengine, yamekuwa yakitekeleza jinai dhidi ya raia.

Kushindwa askari wa serikali na wale wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kukabiliana na waasi hao, inatajwa kuwa sababu kuu ya kushadidi machafuko katika maeneo hayo.

Tags