Jenerali Khalifa Haftar ahimiza kuendelea mapambano dhidi ya magaidi Libya
Mkuu wa vikosi vinavyoitwa Jeshi la Taifa la Libya amesema kuwa jeshi hilo litaendelea na operesheni zake za kupambana na magaidi katika mji wa Derna wa mashariki mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, Jenerali Khalifa Haftar ametangaza kuwa, wanajeshi wake wataukomboa mji wa Derna kutoka mikononi mwa magaidi. Vile vile amewataka wakazi wa mji huo kushirikiana na Jeshi la Taifa la Libya kuwafurusha magaidi hao.
Hii ni katika hali ambayo viongozi wa Libya wameonya juu ya uwezekano wa magaidi kuwatumia raia kama ngao ya kujilinda na mashambulizi. Juzi Jumatatu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliitisha kikao maalumu cha kuchunguza hali ya Libya pamoja na operesheni ya kijeshi katika mji wa Derna. Operesheni ya kuukomboa mji wa Derna ilianza tarehe 7 mwezi huu wa Mei kwa amri ya Khalifa Haftar.

Kwa muda mrefu sasa mji wa Derna wa mashariki mwa Libya unadhibitiwa na kundi linalojiita Baraza la Mujahid wa Derna, ambalo ni moja ya matawi ya mtandao ya kigaidi wa al Qaida huko nchini Libya.
Libya ilitumbukia kwenye machafuko tangu mwaka 2011 wakati wa kampeni za kuung'oa madarakani utawala wa Kanali Muammar Gaddafi. Marekani na nchi za Magharibi ziliivamia kijeshi nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, zikafanya uharibifu wa kupindukia kwenye miundombinu ya nchi hiyo na baadaye kuitelekeza nchi huku silaha zikiwa zimezagaa mikononi mwa makundi hasimu. Tangu wakati huo hadi leo hii Libya haijawahi kushuhudia utilivu hata siku moja kutokana na kila kundi kuendelea kupigania nafasi kubwa zaidi nchini humo.