Serikali ya Cameroon yailalamikia Marekani kwa kuingilia masuala yake ya ndani
Wizara ya mambo ya nje ya Cameroon imemwita balozi wa Marekani nchini humo na kumlalamikia kwa kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo.
Duru za kidiplomasia zimesema kuwa, balozi wa Marekani mjini Yaoundé, Peter Henri Barlerin ameitwa katika wizara ya mambo ya nje ya Cameroon ili kukabidhiwa malalamiko ya nchi hiyo kutokana na kuingilia mambo yasiyomuhusu. Ingawa alichoambiwa hasa Barlerin katika wizara hiyo hakikutangazwa, lakini wachunguzi wanasema kinahusiana na tamko la hivi karibuni la karibuni ya balozi huyo wa Marekani.

Itakumbukwa kuwa siku ya Ijumaa Barlerin alitoa tamko na kusema kuwa serikali ya Cameroon inafanya mauaji na kuwatia mbaroni watu kwa mpangilio maalumu sambamba na kukanyaga haki zao na za familia zao na inafanya uporaji na kuchoma moto mali za wapinzani wa serikali katika maeneo yanayozungumza Kiingereza nchini humo
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya balozi huyo wa Marekani kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Paul Biya wa Cameroon.
Maeneo ya kaskazini magharibi na kusini magharibi mwa Cameroon ni ya wakazi wanaozungumza lugha ya Kiingereza na wanaunda asilimia 20 ya wakazi wote wa nchi hiyo. Wakazi wa maeneo hayo wanalalamikia kubaguliwa na kutengwa na serikali kuu.