May 27, 2024 11:57 UTC
  • Saudia yateua balozi wake nchini Syria baada ya zaidi ya muongo mmoja

Saudi Arabia imetangaza kuteua balozi wake mpya nchini Syria ikiwa ni balozi wake wa kwanza baada ya zaidi ya muongo mmoja tangu ilipositisha uhusiano wake na serikali yar ais Bashar al-Assad.

Hatua hiyo ya Saudi Arabia imetathminiwa na wajuzi wa mambo kuwa ni kiashirio cha utawala wa kifalme wa nchi hiyo kulegeza msimamo wake na kushindwa kampeni yake iliyoianzisha ya kuhakikisha Syria inatengwa na mataifa ya Kiarabu.

Uteuzi wa Faisal al-Mujffal kama balozi wa kwanza wa Saudi Arabia nchini Syria tangu mwaka 2012 ulitangazwa na shirika la habari la Saudi Arabia. Hatua hiyo imekuja ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja tangu Syria ikubaliwe tena katika jumuiya ya nchi 22 wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.

Bendera za Syria na Saudi Arabia

 

Mwaka jana (2023) mataifa mawili ya Saudi Arabia na Syria yalifikia makubaliano ya kurejesha tena uhusiano wao wa kidiplomasia baada ya kupita zaidi ya muongo mmoja tangu Riyadh ilipochukua hatua ya kuvunja uhusiano huo na kuanza kuunga mkono makundi ya kigaidi yaliyokuwa yakipambana na serikali ya Damascus.

Itakumbukwa kuwa Saudi Arabia na washirika wake walivunja uhusiano wao wa kidiplomasia na Syria mwaka 2011 kufuatia kuzuka wimbi kubwa la machafuko na mapigano yaliyoanzishwa na makundi ya kigaidi yakichochewa na kuungwa mkono na muungano wa Magharibi na wa Waarabu dhidi ya taifa hilo la Kiarabu.

Tags