Wahajiri 1,500 waokolewa katika bahari ya Mediterranean
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i44994-wahajiri_1_500_waokolewa_katika_bahari_ya_mediterranean
Takriban wahajiri 1,500 wamenusuriwa wakiwa katika safari hatarishi katika bahari ya Mediterranean, kwenye operesheni zilizofanyika siku ya Alkhamisi na jana Ijumaa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 26, 2018 03:23 UTC
  • Wahajiri 1,500 waokolewa katika bahari ya Mediterranean

Takriban wahajiri 1,500 wamenusuriwa wakiwa katika safari hatarishi katika bahari ya Mediterranean, kwenye operesheni zilizofanyika siku ya Alkhamisi na jana Ijumaa.

Jana Ijumaa pekee, operesheni saba zilizoongozwa na Gadi ya Pwani ya Italia katika bahari hiyo ziliokoa wahajiri 1,050 waliokuwa wakitumia boti dhaifu wakiwa katika jitihada za kwenda kutafuta maisha mazuri barani Ulaya.

Siku ya Alkhamisi, manowari za Italia ziliokoa wahajiri 69 huku meli za kijeshi za Ureno zikiokoa wahajiri wengine 296 siku hiyohiyo.

Libya ndiyo njia kubwa ya wakimbizi wa Kiafrika wanaohatarisha maisha yao katika safari hizo za kutisha za kuelekea barani Ulaya kwa tamaa ya kuwa na maisha mazuri.

Wahajiri wa Kiafrika wakiwa wamejaa katika boti ya plastiki katika bahari ya Mediterranean

Magenge ya biashara haramu za magendo ya wanadamu yanatumia fursa ya kukosekana usalama na serikali kuu yenye nguvu huko Libya kuingiza makumi ya maelfu ya wahamiaji haramu nchini humo kila mwaka, yakiwarubuni kuwa yatawafikisha barani Ulaya salama salmin.

Asilimia kubwa ya wahajiri hao huwa hawafiki wanakokwenda bali imma huzama baharini au hupigwa mnada kama bidhaa masokoni katika biashara ya utumwa mambo leo, na wengine huishia kwenye makucha ya magenge ya kigaidi.