May 28, 2018 14:41 UTC
  • Watu 7 wauawa katika shambulizi la kigaidi karibu na msikiti Nigeria

Kwa akali watu saba wameuawa katika shambulizi la kigaidi lililotokea karibu na msikiti mmoja kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Bello Danbatta, Afisa Mkuu wa Usalama katika jimbo la Borno ameliambia shirika la habari la AFP leo Jumatatu kuwa, magaidi wawili wanawake waliokuwa wamejifunga mabomu pia wameangamia katika shambulizi hilo la jana jioni, karibu na msikiti ulioko katika kijiji cha Konduga, tarafa ya Mashamari, yapata kilomita 53 kusini mashariki mwa Maiduguri, makao makuu ya mkoa wa Borno.

Afisa huyo wa serikali amesema watu watatu waliokuwa wakijiandaa kusali Sala ya Magharibi waliuawa papo hapo kwenye hujuma mbili za mabomu katika eneo hilo.

Moja ya misikiti iliyoshambuliwa katika jimbo la Borno Aprili 25

Naye Ibrahim Liman, askari wa kujitolea ambaye analisaidia jeshi la Nigeria kupambana na wanamagambo wa Boko Haram katika eneo hilo amesema watu wengine wawili walipoteza maisha wakati walipokuwa njiani kuwahishwa hospitalini baada ya kujeruhiwa.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, watu wasiopungua 11 waliuawa huku misikiti miwili ikiteketezwa kwa moto katika jimbo la Benue la katikati mwa Nigeria, siku moja baada ya watu wengine 18 kuuawa wakiwa kanisani katika jimbo hilo.

Tags