Zuma Anusurika kura ya kumwondoa madarakani
Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini amenusurika kura ya kutokuwa na imani naye bungeni.
Jana Bunge la Afrika Kusini lilipinga kura ya kumwondoa madarakani Rais Zuma, lakini mahakama ya katiba imesema alikiuka katiba kwa kukataa kulipa fedha za umma alizotumia kufanyia ukarabati wa nyumba yake binafsi.
Wabunge wa chama tawala cha ANC wamepinga hatua iliyopendekezwa na chama cha upinzani, na kusema Rais Zuma hakukiuka katiba kwa makusudi.
Zuma alipata kura kutoka kwa wabunge 233 wanaomuunga mkono dhidi ya 143 za wabunge ambao hawakuwa na imani naye.
Upinzani uliwasilisha kesi mahakamani baada ya Rais Zuma kupuuza uamuzi wa mwaka 2014 kuwa, alinufaika kutokana na ukarabati wa nyumba yake na kwamba alistahili kulipa pesa zilizotumiwa.
Chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) kinachoongozwa na Julius Malema, aliyeasi ANC, kimekuwa kikimshinikiza Rais Zuma ajiuzulu.