Waafrika wengi hutembelea zaidi bara hilo kuliko kutoka nje yake – Ripoti
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i45294-waafrika_wengi_hutembelea_zaidi_bara_hilo_kuliko_kutoka_nje_yake_ripoti
Uchunguzi uliofanywa na wataalamu wa kimataifa kuhusu faida za wahamiaji kwa nchi wanazotembelea na wanazotoka unaonesha kuwa, asilimia kubwa ya Waafrika wanapenda kutembelea nchi za bara hilo kuliko kutoka nje ya Afrika.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jun 01, 2018 23:40 UTC
  • Waafrika wengi hutembelea zaidi bara hilo kuliko kutoka nje yake – Ripoti

Uchunguzi uliofanywa na wataalamu wa kimataifa kuhusu faida za wahamiaji kwa nchi wanazotembelea na wanazotoka unaonesha kuwa, asilimia kubwa ya Waafrika wanapenda kutembelea nchi za bara hilo kuliko kutoka nje ya Afrika.

Ripoti mpya iliyotolewa na asasi ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa inaonesha kuwa, wahamiaji wamekuwa wakitoa mchango mkubwa katika uzalishaji wa ndani, ajira, biashara, kupunguza umaskini na ustawi wa nchi zao za asili na nchi wanazohamia.

Eneo la mpakani baina ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Ripoti hiyo ya kimataifa imeonesha matokeo ya uchunguzi wa mwaka jana ambao unaonesha kuwa, Waafrika milioni 19 walihamia katika nchi nyingine za Afrika ikilinganishwa na milioni 17 waliokwenda nje ya bara hilo. Zaidi ya hapo watu milioni 5.5 walihamia barani Afrika mwaka huo kutoka nje ya bara hilo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nchi tano za Afrika zilizopokea wahamiaji wengi zaidi mwaka jana ni Afrika Kusini, Kodivaa, Uganda, Nigeria na Ethiopia.

Mchango uliotolewa na wahamiaji katika pato la taifa mwaka 2008 huko Kodivaa ni asilimia 19, Rwanda ni asilimia 13 mwaka 2012, na Afrika Kusini ni asilimia 9 mwaka 2011.

Wahajiri katika mpaka wa Rusumo baina ya Tanzania na Rwanda

Kwa upande wake, Bi Claudia Roethlisberger afisa wa masuala ya uchumi katika kitengo cha bara la Afrika cha nchi zenye maendeleo Madogo na Mipango Maalumu cha Umoja wa Mataifa amesema, ni ngano kudai kuwa wahamiaji wanapunguza ajira. Uchunguzi wetu unaonesha kuwa, wahamiaji wanasaidia sana katika pato la taifa la nchi wanazohamia na wanazotoka.