AU yatakiwa kuongoza mazungumzo ya amani ya Burundi
Mabalozi wa nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika katika Umoja wa Ulaya wameutaka Umoja wa Afrika uingie usukani katika mazungumzo ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa unaozidi kutokota nchini Burundi.
Mabalozi hao wametoa mwito huo huko Kampala, mji mkuu wa Uganda, wiki mbili baada ya Mwenyekiti ya Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat kusema kuwa mazungumzo ya amani ya Burundi yanayoongozwa na viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC, hayajafikia tija yoyote kufikia sasa.
Wakati huo huo, nchi za Umoja wa Ulaya ambazo zimeiwekea vikwazo serikali ya Burundi zimesema mazungumzo hayo ya amani yakiongozwa na AU na Umoja wa Mataifa yumkini yakazaa matunda kwa kuwa asasi hizo mbili zina uwezo wa kufanikisha mchakato huo kwa kutoa suluhu ya kivitendo na kifedha.
Hii ni katika hali ambayo, Alkhamisi iliyopita, Mahakama ya Katiba ya Burundi ilitupilia mbali kesi iliyowasilishwa na muungano wa upinzani nchini humo kupinga matokeo ya kura ya maoni ya kuifanyia marekebisho katiba ya nchi, yaliyoipa ushindi kambi ya serikali, jambo ambalo limeuhamakisha mno upinzani nchini humo.
Kwa mujibu wa matokeo rasmi ya Tume ya Uchaguzi Burundi, asilimia 73 ya wapiga kura milioni 4.3 katika zoezi hilo waliunga mkono kwa kura ya ndio kufanyika marekebisho ya katiba, ambayo yanampa baraka Rais Pierre Nkurunziza kusalia madarakani hadi mwaka 2034.
Nchi hiyo ndogo ya katikati mwa Afrika imekuwa katika mgogoro wa kisiasa tokea Aprili mwaka 2015, baada ya Nkurunziza kugombea muhula wa tatu wa urais ambapo wapinzani walisema ni kinyume cha sheria.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, watu wasiopungua 1,200 wameuawa tokeo wakati huo hadi sasa.