Mgogoro wa Marekani na Rwanda kuhusu nguo za mtumba
Hatua ya serikali ya Rwanda kupiga marufuku nguo za mtumba kutoka Marekani imepelekea kuibuka msuguano baina ya nchi hizo mbili.
Mwezi Machi mwaka huu, Marekani iliipatia Rwanda notisi ya siku 60 ya kupiga marufuku nguo zilizoshonwa katika nchi hiyo ya Afrika kuingizwa Marekani. Rwanda ni kati ya nchi kadhaa za Afrika, ambazo zimekuwa zikiuza nguo mpya Marekani bila kutozwa ushuru katika mpango wa AGOA. Naibu Mwakilishi wa Marekani katika masuala ya Biashara CJ Mahoney amesema Rais Donald Trump ana azma ya kuziadhibu nchi ambazo zinakiuka matakwa ya kibiashara ya Washington.
Pamoja na hayo Rwanda inasisitiza kuwa uingizaji wa nguo za mtumba kutoka Markeani ni jambo ambalo limevuruga viwanda vya nguo katika nchi hiyo.
Rwanda pia inasema haikubali wananchi wake kuvaa tena mitumba kwani huo ni udhalilishaji. Mwaka 2015, nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zilitangza mpango wa kupiga marufuku nguo za mtumba ifikapo mwaka 2019. Hatua hiyo ya EAC inalenga kufufua sekta ya viwanda vya ufumaji nguo vya eneo hilo ambavyo viliwahi kunawiri sana katika miongo ya 70 na 80 kabla ya kuvurugika kutokana na utumizi wa kupindukia wa mitumba.