UN yaelezea wasi wasi wake kuhusu kushtadi kamatakamata Misri
Ofisi ya Kutetea Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imeeleza juu ya wasi wasi mkubwa ilionao kutokana na kushtadi wimbi la kamatakamata nchini Misri.
Msemaji wa ofisi hiyo ya UN, Ravina Shamdasani amesema visa vya watu kukamatwa na kuzuilia kinyume cha sheria nchini Misri ni tatizo lililokolea na linaloonyesha ukiukwaji wa wazi wa haki ya uhuru wa kujieleza, kutangamana na kukusanyika.
Miongoni mwa wanaharakati wa upinzani na wakosoaji wa serikali waliokamatwa hivi karibuni ni mwanablogu Wael Abbas, mchekeshaji maarufu anayeikosoa serikali Shady Abu Zeid na mwanaharakati Amal Fathy.
Msemaji wa Ofisi ya Kutetea Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ametoa matamshi haya siku chache baada ya vyombo vya usalama vya Misri kumtia mbaroni kiongozi mashuhuri wa upinzani nchini humo, Hazim Abdelazim, kwa tuhuma za kuchapisha habari za uongo na kueneza uchochezi dhidi ya dola.
Aidha Februari mwaka huu, mkuu wa chama kingine cha upinzani cha Misri Imara, Abdul Moneim Aboul Fotouh alitiwa mbaroni baada ya kutoa mwito wa kususiwa uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Machi, kulalamikia hatua ya Rais Abdul Fattal al-Sisi ya kumkandamiza kila aliyetangaza nia ya kuchuana naye kwenye uchaguzi huo.
Wanasiasa wengine kadhaa walikamatwa baada ya kutangaza azma yao ya kuchuana na al-Sisi katika uchaguzi huo wa Machi, ikiwa ni muendelezo wa ukandamizaji na mbinyo wanaowekea wapinzani na wakosoaji wa serikali nchini humo.