Bunge la Zimbabwe latupilia mbali mpango wa kumsaili Mugabe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i45746-bunge_la_zimbabwe_latupilia_mbali_mpango_wa_kumsaili_mugabe
Bunge la Zimbabwe limetupilia mbali mpango wa kutaka kumsaili rais wa zamani wa nchi hiyo, Robert Mugabe, kuhusu utendaji wa migodi ya almasi wakati wa uongozi wake.
(last modified 2024-06-10T09:25:34+00:00 )
Jun 12, 2018 07:10 UTC
  • Bunge la Zimbabwe latupilia mbali mpango wa kumsaili Mugabe

Bunge la Zimbabwe limetupilia mbali mpango wa kutaka kumsaili rais wa zamani wa nchi hiyo, Robert Mugabe, kuhusu utendaji wa migodi ya almasi wakati wa uongozi wake.

Bunge la Zimbabwe lilikusudia kumsaili Mugabe kuhusu matamshi yake ambako alisema serikali imenyimwa mapato ya kwa uchache dola bilioni 15 kutoka kwa makampuni yanayofanya kazi kwenye migodi ya almasi huko mashariki mwa nchi hiyo.

Mugabe ambaye amekataa mara mbili kuhudhuria mbele ya Kamati ya Bunge la Zimbabwe, alitakiwa kwenda mbele ya kamati hiyo jana na ingekuwa mara yake ya kwanza kuonekana hadharani tangu alipoondolewa madarakani mwezi Novemba mwaka jana.

Robert Mugabe

Hata hivyo kamati hiyo imesema kuwa, sasa umetupilia mbali takwa la kumsaili Mugabe baada ya kushauriana na Spika wa Bunge la Zimbabwe.

Kamati hiyo ya Bunge la Zimbabwe haikutoa maelezo kuhusu sababu za uamuzi huo.

Takwa la Kamati ya Bunge la kutaka kumsaili Mugabe pia lilikuwa limepingwa na wanasiasa ndani ya chama tawala cha Zanu-PF.