Bemba wa DRC atakama mahakama ya ICC imuachilie baada ya kuondolewa hatiani
Mawakili wa Jean-Pierre Bemba, makamu wa zamani wa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambaye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai wiki iliyopita ilimuondoa hatiani kuhusu jinai za kivita, leo ametaka mahakama hiyo imuachilie huru.
Bemba, 55, ambaye amekuwa katika kizuizi cha ICC tokea mwaka 2008 alipatikana na hatia ya kuhusika na jinai dhidi ya binadamu na kuhukumiwa miaka 18 gerezani mwaka 2016. Mahakama hiyo ilisikiliza rufaa yake na kutoa hukumu Ijumaa kwamba hana hatia na hivyo kutoa pigo kubwa kwa waendesha mashtaka. Majaji wa rufaa walisema Bemba hawezi kubebeshwa lawama ya mauaji na ubakaji wa raia uliotekelezwa na wanajeshi waliokuwa chini ya amri yake.
Wakili wake, Melinda Taylor, ametoa wito kwa majaji kuamuru Bemba aachiliwe huru mara moja ili ajiunge na familia yake nchini Ubelgiji.
Jaji Bertram Schmitt amesema wanatazamia kutoa uamuzi kuhusu ombi hilo siku ya Jumatano.
Kwa kawaida washukiwa huachiliwa huru wakati mahakama inapowaondoa hatiani lakini Bemba anakabiliwa na mashtaka mengine ya kuvuruga mashahidi wakati kesi yake ikiendelea na akipatikana na hatia anaweza kufungwa kifungo cha hadi miaka mitano jela. Wakili wake anasema tayari Bemba amekaa karibu muongo mmoja kizuizini wakati kesi yake ikiendelea na hivyo hata akipatikana na hatia anapaswa kuachuliwa.
Bemba ambaye alikuwa makamu wa rais katika serikali ya mpito ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kati ya Julai 2003 na Disemba 2006, alishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2006 ambapo Kabila aliibuka mshindi.