Rwanda haitasalimu amri mbele ya mashinikizo ya Marekani kuhusu mitumba
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46222-rwanda_haitasalimu_amri_mbele_ya_mashinikizo_ya_marekani_kuhusu_mitumba
Rwanda imesema haitasalimu amri mbele ya Marekani kuhusu uamuzi wake wa kupiga marufuku nguo za mitumba.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 23, 2018 09:17 UTC
  • Rwanda haitasalimu amri mbele ya mashinikizo ya Marekani kuhusu mitumba

Rwanda imesema haitasalimu amri mbele ya Marekani kuhusu uamuzi wake wa kupiga marufuku nguo za mitumba.

Hayo yamedokezwa Waziri wa Mambo ya Nje  wa Rwanda Olivier Nuhungirehe ambaye ameongeza kuwa nchi yake itanshikilia msimamo wa kupiga marufuku nguo za mitumba ili kuhimiza utumizi wa bidhaa zilizotengenezwa Rwanda.

Amesema Rwanda haina wasiwasi iwapo itaondolewa katika mpango wa Marekani wa Ukuzaji Fursa za kiuchumi Afrika (AGOA). Amesema Rwanda inataka kuimarisha sekta ya viwanda vya ufumaji nguo na kwa msingi huo hairuhusu tena mitumba nchini humo.

Mwezi Machi mwaka huu, Marekani iliipatia Rwanda notisi ya siku 60 ya kupiga marufuku nguo zilizoshonwa katika nchi hiyo ya Afrika kuingizwa Marekani. Rwanda ni kati ya nchi kadhaa za Afrika, ambazo zimekuwa zikiuza nguo mpya Marekani bila kutozwa ushuru katika mpango wa AGOA. Naibu Mwakilishi wa Marekani katika masuala ya Biashara CJ Mahoney amesema Rais Donald Trump ana azma ya kuziadhibu nchi ambazo zinakiuka matakwa ya kibiashara ya Washington.

Rais Trump wa Marekani

Mwaka 2015, nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zilitangaza mpango wa kupiga marufuku nguo za mtumba ifikapo mwaka 2019. Hatua hiyo ya EAC inalenga kufufua sekta ya viwanda vya ufumaji nguo vya eneo hilo ambavyo viliwahi kunawiri sana katika miongo ya 70 na 80 kabla ya kuvurugika kutokana na utumizi wa kupindukia wa mitumba.