DRC kumpa Bemba pasipoti ya kidiplomasia, kumruhusu arejee nyumbani
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imesema itampa pasipoti ya kidiplomasia Makamu wa Rais wa zamani wa nchi hiyo ambaye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ilimuondoa hatiani hivi karibuni.
Kwa mujibu wa nakala ya barua ya Leonard She Okitundu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kongo DR kwa Spika wa Seneti ya nchi hiyo, serikali inataka Jean-Pierre Bemba apewe pasi ya kidiplomasia kupitia ubalozi wa DRC mjini Brussels na kuruhusiwa arejee nyumbani.
Chama cha Bemba cha Movement for the Liberation of Congo kimesema mwanasiasa huyo angali Katibu Mkuu wake na kinamtarajia katika mkutano mkuu wa chama hicho cha upinzani mapema mwezi ujao.
Baada ya kuondolewa lawamani na kuachiwa huru na ICC siku chache zilizopita, Bemba aliekekea Ubelgiji kujiunga na familia yake inayoishi katika eneo la Rhode-Saint-Genese, yapata kilomita 15 kusini mwa mji mkuu wa nchi hiyo Brussels, eneo ambako alikamatwa Mei 2008, kufuatia ombi la ICC.
Bemba mwenye umri wa miaka 55, ambaye amekuwa katika kizuizi cha ICC tokea mwaka 2008 alipatikana na hatia ya kuhusika na jinai dhidi ya binadamu na kuhukumiwa kifungo cha miaka 18 gerezani mwaka 2016.
Siku chache zilizopita mahakama hiyo iliyoko mjini The Hague nchini Uholanzi ilisikiliza rufaa ya Bemba na kutoa hukumu kwamba hana hatia, na kusisitiza kuwa hawezi kubebeshwa lawama ya mauaji na ubakaji wa raia uliofanywa na wanajeshi waliokuwa chini ya amri yake.