Wapinzani Malawi wamtaka Rais Mutharika ajiuzulu kutokana na madai ya ufisadi
Chama kikuu cha upinzani nchini Malawi leo kimemtaka Rais Peter Mutharika wa nchi hiyo ajiuzulu kufuatia madai kuwa alipokea fedha haramu katika mkataba wa serikali wa dola milioni nne.
Mutharika ameyataja madai hayo kuwa ni "taarifa za uwongo" zilizobuniwa kumchafulia jina kabla ya uchaguzi wa mwakani. Lazarus Chakwera kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Congresi ya Malawi amesema kuwa chama hicho kipo pamoja na makundi ya kiraia ya nchi hiyo wakimtaka Rais Mutharika ajiuzulu. Amesema Rais Peter Mutharika anapasa kujiuzulu na kuitisha uchaguzi wa mapema. Itafahamika kuwa Idara ya Kupambana na Ufisadi ya Malawi imekuwa ikichunguza mkataba wenye thamani ya dola milioni 3.8 wa kusambaza chakula kwa polisi wa nchi hiyo ambao zabuni yake ilitolewa kwa Kampuni ya Pioneer Investments inayomilikiwa na mfanyabishara Zameer Karim. Mfanyabiashara huyo amekanusha kuhusika katika ufisadi uliotajwa.

Taarifa iliyovuja imebainisha kuwa mfanyabiashara huyo aliweka katika akaunti ya chama tawala kiasi cha kwacha milioni 145 za Malawi sawa na dola laki mbili; akaunti ambayo ni Mutharika pekee ndiye mwenye dhamana ya kutia saini. Madai ya mara kwa mara ya ufisadi yanayoikabili serikali ya Rais Mutharika huenda yakakwamisha kampeni zake kuelekea katika uchaguzi mkuu wa mwakani. Chaguzi za rais, bunge na mitaa nchini Malawi zimepangwa kufanyika mwezi Mei mwaka kesho.