9 waaga dunia katika ajali iliyotokea katika barabara ya Nairobi-Mombasa, Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46557-9_waaga_dunia_katika_ajali_iliyotokea_katika_barabara_ya_nairobi_mombasa_kenya
Watu tisa wamepoteza maisha katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea mapema leo katika barabara kuu ya Nairobi kuelekea Mombasa nchini Kenya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 04, 2018 03:10 UTC
  • 9 waaga dunia katika ajali iliyotokea katika barabara ya Nairobi-Mombasa, Kenya

Watu tisa wamepoteza maisha katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea mapema leo katika barabara kuu ya Nairobi kuelekea Mombasa nchini Kenya.

Basi la kampuni ya Mombasa ya BusCar limeteketea moto baada ya kugongana ana kwa ana na lori kati ya mji wa Emali na Sultan Hamud katika kauti ya Makueni kusini mwa nchi.

Mohammed Maalim, Kamishna wa Kaunti ya Makueni amethibitisha kuwa watu tisa wamepoteza maisha katika ajali hiyo huku wengine 20 wakijeruhiwa na kupelekwa katika Hospitali ya Kilome kwa ajili ya matibabu.

Waliofariki dunia katika ajali hiyo wamepelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Makindu.

 

Basi lililoripuka na kuteketea baada ya ajali Kenya

Naye Paul Odede, Mkuu wa Polisi katika eneo la Kilungu amesema abiria 10 kati ya 39 waliokuwa kwenye basi hilo wamekwama kwenye mabaki ya basi hilo, huku kukiwa na wasiwasi kuwa yumkini wameteketea hadi kuwa majivu.

Makumi ya watu hupoteza maisha kila mwaka katika ajali zinazotokea mara kwa mara katika eneo hatari la barabara hiyo ya Nairobi-Mombasa, baina ya mji wa Emali na Sultan Hamud kaunti ya Makueni, hususan nyakati za usiku.