10 wauawa kwa kuchomwa moto katika machafuko ya kikabila Kongo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46646-10_wauawa_kwa_kuchomwa_moto_katika_machafuko_ya_kikabila_kongo_dr
Watu kumi wameuawa kwa kuteketezwa moto katika ghasia za kikabila zilizojiri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 08, 2018 09:10 UTC
  • 10 wauawa kwa kuchomwa moto katika machafuko ya kikabila Kongo DR

Watu kumi wameuawa kwa kuteketezwa moto katika ghasia za kikabila zilizojiri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Miili iliyosalia majivu ya kumi hao imepatikana katika eneo la Kivu Kusini, baada ya kujiri makabiliano makali baina ya makundi matatu ya kikabila, ya Banyamulenge, Bafuliro na Banyindu.

Afisa mkuu wa eneo la Tanganyika,  John Mwimiwa amesema watu wa kabila la Banyamulenge (Watutsi wa Kongo) huwa wanatizamwa kama wageni wavamizi na makabila mawili ya Bafuliro na Banyindu na makundi hayo yamekuwa yakishambuliana mara kwa mara katika mkoa wa Kivu, mashariki mwa DRC.

Eneo la mashariki nchini DRC limekuwa likishuhudia mauaji na machafuko kwa miaka mingi

Afisa huyo ameongeza kuwa, hapo jana Jumamosi kulijiri pia mapigano baina ya waasi wa makundi ya Ngumino na Forebu katika wilaya za Uvira na Fizi, ambapo watu kadhaa walijeruhiwa mbali na vijiji kadhaa kuchomwa moto.

Katika hatua nyingine, Mak Hazukay, msemaji wa Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema askari mmoja wa nchi hiyo ameuawa, huku raia mmoja akijeruhiwa, baada ya kushambuliwa na waasi wa Uganda wa ADF Nalu, katika mkoa wa Beni, mashariki mwa DRC.