Jeshi la Misri laangamiza magaidi 11 Peninsula ya Sinai
Jeshi la Misri limetangaza habari ya kuua wanachama 11 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) katika eneo la Sinai, kaskazini mwa nchi.
Shirika rasmi la habari la Misri MENA limetangaza habari hiyo leo Jumatano na kuongeza kuwa, maafisa usalama wa Misri wameshambulia maficho ya magaidi hao katika mji wa al-Arish na kuwaangamiza magaidi hao.
Hata hivyo vyanzo vya habari vilivyonukuliwa na shirika hilo la habari havijasema ni lini au ni wapi haswa kulikotokea makabiliano hayo mjini al-Arish.
Mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu, magaidi wengine wanane na askari wawili wa Misri waliuawa katika makabiliano yaliyotokea katika Rasi ya Sinai. Hujuma hiyo ilifanyika wiki mbili baada ya Jeshi la Misri kutangaza habari ya kuangamizwa magaidi 19 katika operesheni iliyofanywa na jeshi la nchi hiyo katika Peninsula ya Sinai.
Mwezi Februari mwaka huu, jeshi la Misri kwa kushirikiana na polisi lilianzisha operesheni ya pamoja inayojulikana kwa jina la 'Sinai 2018' kwa shabaha ya kuyasafisha magenge ya kigaidi katika eneo hilo la kaskazini mwa nchi.
Duru za habari zimeeleza kuwa, magaidi wasiopungua 280 wameshauawa tangu ilipoanza operesheni hiyo, na watu 4467 wameshatiwa mbaroni. Kadhalika jeshi la Misri limepoteza askari wake karibu 40 katika operesheni hiyo.