Maandamano dhidi ya chama tawala yafanyika Zimbabwe
Maelfu ya wafuasi wa upinzani jana Jumatano walijitokeza mabarabarani kushiriki maandamano dhidi ya chama tawala nchini Zimbabwe Zanu-pf katika mji mkuu Harare.
Waandamanaji hao wanataka kufanyika uchaguzi huru na wa haki, huku kukiwa na tetesi za kupangwa njama na maafisa wa tume ya uchaguzi ya kuiba kura kwa niaba ya chama tawala.
Waandamanaji hao waliokuwa wamevalia kofia na fulana zenye picha za mwanasiasa barobaro, Nelson Chamisa, wamesema wamechoshwa na uongozi wa miongo kadhaa wa chama tawala cha Zanu-pf.
Waandamanaji hao wakiongozwa na Chamisa wameikabidhi Tume ya Kitaifa ya Uchaguzi barua yao ya malalamiko, wakiitaka iendeshe zoezi hilo kwa uadilifu na kwa kuzingatia kanuni za tume na sheria za nchi.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, polisi ya Zimbabwe ilimtia mbaroni Dakta Francis Danha, kinara wa chama cha upinzani cha Freedom Movement, akiwa katika mkutano wa vyama vya upinzani, ambapo alitoa mwito wa kujiuzulu Priscilla Chigumba, Mkuu wa Tume ya Kitaifa ya Uchaguzi nchini humo NEC.
Mwanasiasa huyo alikamatwa siku chache baada ya Rais Emmerson Mnangagwa kuponea chupuchupu katika mripuko uliotokea katika mkutano wake wa kisiasa mjini Bulawayo. Mnangagwa ambaye alirithi mikoba ya mtangulizi wake Robert Mugabe, anatazaiwa kugombea kiti cha urais katika uchaguzi mkuu ujao unaotazamiwa kufanyika Julai 30.