Watu 16 wapoteza maisha katika ajali ya boti Tshopo, DRC
Watu 16 wamethibitishwa kupoteza maisha kufuatia ajali ya boti katika Mto Kongo ulio mkoa wa Tshopo kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mkuu wa mkoa huo, Jean Ilongo Tokole alitangaza Ijumaa kuwa, watu wengine 34 hadi sasa hawajulikani waliko huku wengine 100 wakiwa wamenusurika baada ya ajali hiyo kutokea Jumanne usiku. Kufuatia ajali hiyo usafiri wa boti wakati wa usiku katika eneo hilo umesimamishwa kwa muda.
Imedokezwa kuwa boti hiyo ya abiria na mizigo ilikuwa ikisafiri kutoka Lokutu hadi Kisangani, mji mkuu wa mkoa wa Tshopo. Taarifa zinasema boti hiyo ilikuwa ikisafiri usiku bila mataa wakati ilipopata ajali yapata kilomita 200 kutoka Kisangani.

Ajali za boti hujiri mara kwa mara ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutokana na boti zilizoharibika kutumiwa katika usafiri na pia kutokana na kubeba mizigo au abiria kupita kiasi.