Katumbi kurejea DRC wiki hii kwa lengo la kuwania urais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i47143-katumbi_kurejea_drc_wiki_hii_kwa_lengo_la_kuwania_urais
Billionea na mwanasiasa wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Moise Katumbi amesema anaomba ruhusu ya kurudi nyumbani wiki hii, kwa lengo la kuwania urais mwezi Desemba.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jul 31, 2018 11:21 UTC
  • Katumbi kurejea DRC wiki hii kwa lengo la kuwania urais

Billionea na mwanasiasa wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Moise Katumbi amesema anaomba ruhusu ya kurudi nyumbani wiki hii, kwa lengo la kuwania urais mwezi Desemba.

Katumbi ambaye amekuwa akiishi nchini Ubelgiji, amesema kwa sasa yupo jijini Johannesburg Afrika Kusini na tayari ameliandikia barua shirika la safari za anga nchini humo kumruhusu arejee nyumbani kwa kutumia ndege yake binafsi.

Gavana huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 53, alikimbilia uhamishoni mwaka 2016 baada ya kuhitilafiana kisiasa na rais Joseph Kabila.

Hata hivyo, ripoti zinasema kuwa iwapo Katumbi atarejea nchini humo hataruhusiwa kuwania kiti cha rais kwa sababu sheria za uchaguzi zinamtaka anayetaka kuwa rais awe ndani ya nchi hiyo kwa angalau mwaka mmoja.

Jean Pierre Bemba

Hayo yanajiri baada ya Makamu wa Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambaye mwezi Mei mwaka huu aliondolewa mashitaka na kuachiwa huru na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), kutangaza kuwa atarejea nyumbani kuwania urais.

Eve Bazaiba, Katibu Mkuu wa chama kikuu cha upinzani cha Movement for the Liberation of Congo (MLC) chake Jean-Pierre Bemba amesema, "Bemba atarejea nyumbani Agosti Mosi, maandalizi yote yanaendelea vizuri."

Uchaguzi mkuu nchini DRC unatazamiwa kufanyika Disemba 23 mwaka huu.