Serikali ya DRC yamzuia kinara wa upinzani, Katumbi, kurejea na kushiriki uchaguzi
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetoa taarifa rasmi kwa Moise Katumbi, mwanasiasa wa upinzani aliye uhamishoni kwamba imekataa suala la kurudi kwake nchini humo. Moise Katumbi alikuwa ametangaza kuwa atarudi nyumbani Ijumaa hii, Agosti 3.
Gavana wa zamani wa Katanga alikua amepanga kurudi nchini kwake kupitia Lubumbashi ili kuchukua fomu ya kuwania katika uchaguzi wa urais, lakini hajapewa ruhusa ya ndege yake binafsi kutua katika ardhi ya DRC. Hata hivyo Moise Katumbi na washirika wake wanasema watapuuza marufuku hiyo.
Moise Katumbi alitangaza kwamba atawasili Lubumbashi Ijumaa asubuhi, Agosti 3, lakini ndege yake binafsi haijapewa ruhusa ya kutua. Katika barua, meya wa Lubumbashi, Ghislain Robert Lubaba Buluma amesema ndege hiyo imekataliwa kutua au kupaa katika anga ya DRC kutokana mashtaka yanayoendelea kumkabili Moise Katumbi.
Siku ya Alhamisi, ofisi ya mashtaka ilitangaza kwamba Moise Katumbi atakamatwa baada ya kuwasili nchini DRC kwa kosa la kuhatarisha usalama wa taifa. "Moise Katumbi anakabiliwa na mashtaka ya kuajiri askari mamluki kwa lengo la kuangusha utawala wa Rais Joseph Kabila", vyanzo kadhaa vya serikali vimebaini.
Moise Katumbi anataka kurudi DRC ili kuchukua fomu ya kuwania katika uchaguzi wa urais wa Desemba 23, 2018. Tayari kiongozi mwingine wa upinzani, Jean-Pierre Bemba ambaye alirejea nyumbani Jumatano kutoka Ubelgiji ameshajaza fomu za kuwania urais.
Wapinzani wanamtuhumu Rais wa sasa Joseph Kabila kuwa anapanga kuwania urais kinyume cha katiba katika hali ambayo muhula wake ulimalizika Disemba 2017 baada ya kuwa madarakani kwa kipindi cha miaka 17. Kabila ameendelea kushikilia madaraka kwa kutumia kipengee cha katiba kinachomruhusu kuendelea kutawala hadi rais mwingine atakapochaguliwa.