Wananchi wa Libya waandamana kulalamikia maisha magumu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i47246-wananchi_wa_libya_waandamana_kulalamikia_maisha_magumu
Miji mingi ya Libya imekumbwa na maandamano ya wananchi wanaolalamikia maisha magumu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 05, 2018 10:48 UTC
  • Wananchi wa Libya waandamana kulalamikia maisha magumu

Miji mingi ya Libya imekumbwa na maandamano ya wananchi wanaolalamikia maisha magumu.

Mtandao wa habari wa al Yaum al Saabii umeripoti habari hiyo na kusema kuwa wananchi wanaoandamana huko Libya wanataka kutatuliwa haraka mgogoro wa kiuchumi, kuboreshwa maisha yao na kukabiliana na matatizo ya mara kwa mara kama ya kukatika ovyo umeme, kuadimika mikate na kuongezea kiholela bei za bidhaa.

Wananchi wanaoandamana mjini Benghazi wametaka kutoongezewa muda majopo ya kisiasa yanayoongoza masuala ya nchi kutokana na ufisadi mkubwa.

Libya ina migogoro mingi ukiwemo wa kupigwa mnada watu na kuuzwa kama watumwa masokoni 

 

Mjini Misrata pia, waandamanaji wametaka wahalifu wanaofanya kazi ndani ya taasisi za usalama za Libya wakabidhiwe mikononi mwa vyombo vya sheria.

Kwa upande wao, wananchi walioandamana mjini Zawiya wametaka kuendeshwe vita vya kweli vya kupambana na magendo na magenge ya uhalifu wa kibenki.

Tangu mwaka 2011 hadi hivi sasa, Libya haijawahi kushuhudia utulivu hata siku, hususan baada ya Marekani na shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO kuivamia kijeshi Libya katika kampeni ya kumg'oa madarakani Kanali Muammar Gaddafi. Hivi sasa Libya ina serikali mbili na mabunge mawili tofauti huko Tobruk na Tripoli. Machafuko hayo yametoa mwanya kwa magenge ya kigaidi hasa Daesh kufanya vitendo vya kigaidi katika maeneo tofauti ya nchi hiyo kaskazini mwa Afrika.