Rwanda na Burundi zashirikiana katika kuzuia ugonjwa hatari wa Ebola
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i47301-rwanda_na_burundi_zashirikiana_katika_kuzuia_ugonjwa_hatari_wa_ebola
Serikali za Rwanda na Burundi zimeweka mikakati kabambe ya pamoja kwa ajili ya kupambana na maradhi hatari ya Ebola ambayo yameripotiwa katika eneo la Maziwa Makuu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 08, 2018 00:13 UTC
  • Rwanda na Burundi zashirikiana katika kuzuia ugonjwa hatari wa Ebola

Serikali za Rwanda na Burundi zimeweka mikakati kabambe ya pamoja kwa ajili ya kupambana na maradhi hatari ya Ebola ambayo yameripotiwa katika eneo la Maziwa Makuu.

Taarifa iliyotolewa na serikali ya Burundi imesema kuwa, kwa sasa nchi mbili zinafanya ukaguzi mkali kwa wageni wote wanaoingia na kutoka katika mipaka ya nchi hizo. Wizara ya Afya nchini Burundi imesema kuwa serikali ya Bujumbura imeweka mikakati maalumu yenye lengo la kuona kwamba kila mgeni anayeingia nchini humo anakaguliwa afya yake kuhakikisha kuwa hana maradhi hayo. Imesisitiza kuwa, Burundi imejipanga kuhakikisha inakabiliana na janga hilo haraka iwezekanavyo na bila kusita. Pia imepongeza ushirikiano bora wa Shirika la Afya Duniani (WHO) katika juhudi hizo za kukabiliana na Ebola.

Juhudi za kuzuia maambukizi ya maradhi hayo hatari

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, WHO limekuwa mstari wa mbele katika kupambana na kuzuia janga hilo hatari ambalo linaendelea kutishia afya na uhai wa wakazi wa nchi hizo mbili. Wizara ya Afya ya Burundi imeongeza kwamba, maafisa wa afya wa WHO wamekuwa wakishirikiana na maafisa wa Burundi na Rwanda na kwamba tayari magari maalumu yamepelekwa katika vituo vitatu muhimu katika mipaka ya nchi hizo.

Hivi karibuni pia Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitoa taarifa likisema kuwa, hali mpya ya maambukizi ya ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) inazilazimisha nchi za jirani kuchukua hatua za tahadhari ili kuzuia ungojwa huo hatari kusambaa zaidi. Aidha WHO ilisema kukabiliana na mlipuko mpya wa Ebola nchini DRC si kazi rahisi.