Tunisia yakosoa uingiliaji kati wa nchi ajinabi huko Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i47302-tunisia_yakosoa_uingiliaji_kati_wa_nchi_ajinabi_huko_libya
Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia ameeleza wasiwasi wake kuhusu hali ya machafuko inayoendelea kushuhudiwa nchini Libya na kusema kuwa nchi hiyo imekuwa medani ya vita vya niaba vya pande za kigeni.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Aug 08, 2018 02:14 UTC
  • Tunisia yakosoa uingiliaji kati wa nchi ajinabi huko Libya

Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia ameeleza wasiwasi wake kuhusu hali ya machafuko inayoendelea kushuhudiwa nchini Libya na kusema kuwa nchi hiyo imekuwa medani ya vita vya niaba vya pande za kigeni.

Khemaies Jhinaoui ameutaja uingiliaji kati wa jeshi wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (Nato) huko Libya kuwa ni haribifu kwa nchi hiyo na kwa majirani zake na kwamba hatua hiyo inazidisha ukosefu wa amani na hali ya mchafukoge huko Libya. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia ameongeza kuwa madola ya kigeni yameifanya nchi ya Libya kuwa medani ya vita vinavyopiganywa kwa niaba yao na Libya na nchi jirani ndizo zinazopata madhara kutokana na hali ya ndani ya nchi hiyo.  

Taathira za uingiliaji kati kijeshi nchini Libya 

Al Jhinaoui ameashiria pia uingiliaji kati wa Marekani na Uingereza na nchi nyingine za Magharibi katika vita vya ndani nchini Libya na kueleza kuwa nchi hizo ziliishambulia Libya na sasa zimeitelekeza. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia ameongeza kuwa Libya ni nchi yenye utajiri mkubwa wa maliasili lakini uvamizi wa nchi ajinabi umeifanya hali ya mambo nchini humo kuwa ngumu.