Libya yaiomba Russia iisaidie kutatua migogoro yake
Msemaji wa Jeshi la Taifa la Libya ameiomba serikali ya Russia iingilie mgogoro wa Libya kwa ajili ya kuutatua.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Sputnik, Ahmed al Mismari, msemaji wa Jeshi la Taifa la Libya amesema, utatuzi wa mgogoro wa nchi hiyo unahitajia msaada wa Russia na hasa wa Rais Vladimiri Putin mwenyewe wa nchi hiyo.
Amesema, kuna wajibu kwa nchi zilizo na mkono katika mgogoro wa Libya hasa Uturuki, Qatar na Italia kujitoa katika mgogoro huo ndipo utaweza kutatuliwa. Hata hivyo amasema, kuna wajibu wa kutumiwa uzoefu wa kidiplomasia wa Russia kutatua mgogoro wa nchi hiyo.
Ahmed al Mismari amegusia pia ziara ya hivi karibuni ya Jenerali Khalifa Haftar, kamanda wa vikosi vya Jeshi la Taifa la Libya huko Moscow na kusisitiza kuwa, jeshi hilo litaendeleza uhusiano wake na Russia.
Libya ilitumbukia kwenye machafuko mwaka 2011 baada ya Marekani na shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO kuivamia kijeshi nchi hiyo katika kampeni za kuungasha utawala wa Kanali Muammar Gaddafi.
Tangu wakati huo hadi hivi sasa nchi hiyo imeshindwa kuwa na utulivu wa angalau siku na mivutano baina ya makundi mbalimbali yanayoungwa mkono na madola ajinabi ni sababu kuu ya kukosekana utulivu huko Libya.