Wagombea 23 kuchuana DRC kwa ajili ya kumrithi Rais Joseph Kabila
Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza kuwa, wagombea 23 wanatarajiwa kuchuana ili kuwania kumrithi Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo.
Corneille Nangaa, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (CENI) ametangaza kuwa, wagombea hao 23 wanatarajiwa kuchuana katika uchaguzi ujao wa Disemba 23 kuwania kiti cha urais.
Kwa muujibu wa Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo, katika orodha hiyo yumo pia mwanamke mmoja.
Chama tawala cha Rais Kabila cha PPRD hivi karibuni kilimtangaza Emmanuel Ramazani Shadary kuwa mgombea wake katika uchaguzi huo.
Emmanuel Shadari mwenye umri wa miaka 57 ni mwandani wa karibu wa Rais Joseph Kabila na alikuwa katibu wa kudumu wa chama tawala cha PPRD na mtu muhimu wa kampeni za rais Kabila. Wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Shadary alijulikana kuwa mtu asiye na huruma.
Hata hivyo licha ya kuweko orodha hiyo ndefu ya wagombea wa kiti cha urais, wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, mchuano mkali unatarajiwa kuwa kati ya mgombea wa chama tawala Emmanuel Ramazani Shadary na Jean Piere Bemba Makamu wa zamani wa Rais.
Baadhi ya wagombea wengine mashuhuri ni Felix Tshisekedi, kiongozi wa chama cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS) na Tryphon Kin-Kiey Mulumba aliyewahi kuwa msemaji wa Mobutu Sese Seko, rais wa zamani wa nchi hiyo.