Watu 12 wauawa katika mapigano kati ya makundi yenye silaha Kongo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i47370-watu_12_wauawa_katika_mapigano_kati_ya_makundi_yenye_silaha_kongo_dr
Watu 12 wameuawa katika mapigano kati ya makundi yanayobeba silaha yaliyotokea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Aug 11, 2018 03:10 UTC
  • Watu 12 wauawa katika mapigano kati ya makundi yenye silaha Kongo DR

Watu 12 wameuawa katika mapigano kati ya makundi yanayobeba silaha yaliyotokea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Maafisa katika mji wa Goma, makao makuu ya mkoa wa Kivu Kaskazini mashariki mwa Kongo DR wametangaza kuwa watu hao ambao ni raia wa kawaida wameuawa katika mapigano yaliyozuka katika kipindi cha siku tano zilizopita kati ya makundi yanayobeba silaha.

Kwa mujibu wa maafisa hao mapigano hayo yalihusisha kundi la waasi liitwalo Muungano wa Wazalendo kwa ajili ya Kongo Huru na Yenye Kujitawala na lile la Maï-Maï Nduma la Ulinzi wa Kongo.

Wanamgambo wa kundo la waasi la Maï-Maï

Mapigano kati ya makundi hayo mawili ya waasi yameendelea kwa kipindi cha siku tano zilizopita na kuwafanya raia wakimbilie kandokando ya kitongoji cha Masisi mkoani Kivu Kaskazini kutafuta hifadhi.

Kwa muda wa miaka 20 sasa, maeneo ya kati, mashariki na kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamekuwa yakishuhudia mapigano na machafuko yanayosababishwa na makundi ya waasi.

Kushindwa jeshi la serikali ya Kongo DR na vikosi vya Umoja wa Mataifa kukabiliana na makundi ya wanamgambo wanaobeba silaha kumepelekea kushamiri machafuko na mapigano nchini humo.../