Jumuiya za kutetea haki za binadamu: Serikali ya al Sisi inakandamiza wapinzani
(last modified Fri, 17 Aug 2018 03:49:53 GMT )
Aug 17, 2018 03:49 UTC
  • Jumuiya za kutetea haki za binadamu: Serikali ya al Sisi inakandamiza wapinzani

Jumuiya saba za kutetea haki za binadamu nchini Misri zimeikosoa serikali ya nchi hiyo zikisisitiza kuwa mienendo yake dhidi ya wapinzani inakiuka sheria.

Taarifa iliyotolewa na jumuiya hizo kwa mnasaba wa kutimia miaka 5 baada ya mauaji ya waandamanaji katika medani za Rabia na al Nahdha mjini Cairo hapo Agosti mwaka 2013, imesema kuwa suala la kuwapa kinga na kuwakingia kifua wahalifu na kuwahukumu watu wasio na hatia yoyote limekuwa "sheria isiyo rasmi" nchini Misri katika miaka mitano iliyopita. 

Taarifa hiyo imesema kuwa, jinai zilizofanyika medani za Rabia na al Nahdha tarehe 14 Agosti mwaka 2013 bado zimenyamaziwa kimya na watendaji wa mauaji hayo ya kutisha hawajachukuliwa hatua yoyote. 

Tarehe 14 Agosti mwaka 2013 na baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyoindoa madarakani serikali iliyokuwa imechaguliwa na wananchi kwa njia za kidemokrasia, jeshi la Misri likiongozwa na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Rais wa sasa wa nchi hiyo, Abdul Fattah al Sisi lilishambulia waandamanaji katika medani za Rabia al Adawiyya na al Nadha mjini Cairo na kuua mamia ya raia wasio na hatia. 

Jenerali Abdul Fattah al Sisi

Mwezi uliopita wa Julai pia Jenerali Abdul Fattah al Sisi alipasisha sheria inayowapa kinga makamanda wa jeshi la Misri waliohusika na matukio ya kuanzia Julai 2013 hadi Januari mwaka 2016.    

Tags