Wapinzani waitisha maandamano ya nchi nzima DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i47612-wapinzani_waitisha_maandamano_ya_nchi_nzima_drc
Wapinzani wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanataka kusitumike mashine za kupigia kura katika uchaguzi ujao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 22, 2018 09:56 UTC
  • Wapinzani waitisha maandamano ya nchi nzima DRC

Wapinzani wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanataka kusitumike mashine za kupigia kura katika uchaguzi ujao.

Harakati ya kuipinga serikali inayojiita "Mapambano kwa ajili ya Mabadiliko" jana ilizungumza na waandishi wa habari katika miji mingi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ukiwemo mji mkuu Kinshasa na kutangaza kupinga mpango wa kutumika mashine maalumu za kupigia kura na kusema inawataka wafuasi wake wafanye maandamano ya nchi nzima tarehe tatu mwezi ujao wa Septemba na wakusanyike katika ofisi za tume ya uchaguzi katika miji hiyo ili kulazimisha kuondolewa mashine hizo katika mchakato wa upigaji kura.

Zoezi la upigaji kura DRC

 

Malalamiko hayo yametolewa katika hali ambayo, Rais Joseph Kabila amesema kuwa hatobadilisha katiba na hatogombea urais katika uchaguzi ujao.

Hata hivyo maandamano ya harakati ya "Mapambano kwa ajili ya Mabadiliko" yamekuwa yakipigwa marufuku mara kwa mara.  Maafisa wa kulinda usalama wa DRC wamekuwa wakichukua hatua mbalimbali za kukabiliana na waandamanaji.

Wapinzani wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanasema kuwa, mashine hizo zilizotengenezwa Korea Kusini ni "mashine za uchakachuaji" na kwamba mpango wa kutumia mashine hizo katika uchaguzi hauna nia nyingine isipokuwa kuibeba serikali katika uchaguzi.

Mashine hizo hutumika kuchapisha karatasi za kupigia kura na kuchagua wagombea.

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)