Waasi wa ADF- Nalu washambulia jeshi la Kongo mashariki mwa nchi
Duru za kijeshi na za kiraia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimeetangaza kuwa waasi wa Uganda kwa jina la ADF- Nalu wameshambulia kitengo kimoja cha vikosi vya jeshi la Kongo mashariki mwa nchi hiyo.
Watu walioshuhudia katika mji wa Beni mkoani Kivu ya Kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameeleza kuwa karibu waasi 10 wameuawa katika shambulio hilo la waasi wa ADF-Nalu dhidi ya vikosi vya jeshi la Kongo. Waasi wa Uganda walianzisha harakati zao mashariki mwa Kongo tangu mwaka 1994 na katika miaka hiyo yote wameuwa mamia ya raia wa eneo hilo.
Maeneo ya katikati, mashariki na kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yanakabiliwa na ukosefu wa amani kwa miaka 20 sasa. Kushindwa jeshi la Kongo na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kukabiliana na waasi na makundi ya wanamgambo wenye silaha kumepelekea kuongezeka hali ya mchafukoge na ukosefu wa amani nchini humo.