Benki ya Dunia yaipatia mkopo wa dola bilioni moja Ethiopia ili kuendeleza mageuzi
Waziri Mkuu wa Ethiopia amesema kuwa, Benki ya Dunia imeipatia nchi hiyo mkopo wa dola bilioni moja ili kusaidia juhudi za nchi yake za kufanya mageuzi ya kiuchumi na kisiasa.
Abiy Ahmed amebainisha kuwa, katika kipindi cha miezi michache ijayo, Benki ya Dunia itaipatia Ethiopia kifurushi cha kusaidia bajeti ya Addis Ababa cha dola bilioni moja.
Tangu Waziri Mkuu mpya wa Ethiopia aingie madarakani Aprili mwaka huu amefanya mageuzi makubwa ya kisiasa na kiuchumi ambayo yamepokelewa kwa mikono miwili na wananchi wa nchi hiyo.
Mageuzi hayo ya kisiasa na kiuchumi ya Waziri Mkuu wa Ethiopia yamezivutia nchi na taasisi nyingi ikiwemo Benki ya Dunia ambayo imechukua uamuzi wa kuipiga jeki kifedha nchi hiyo ili iweze kusukuma mbele gurudumu lake la mageuzi ya kisiasa na kiuchumi.

Itakumbukwa kuwa, serikali ya Ethiopia iliyaondoa makundi matatu ya upinzani katika orodha ya 'makundi ya kigaidi', ikiwa ni katika muendelezo wa hatua za mageuzi zinazochukuliwa na Waziri Mkuu wa sasa, Abiy Ahmed.
Makundi hayo yaliyokuwa yakipigania kujitenga ni ya Oromo Liberation Front na Ogaden National Liberation Front pamoja na kundi la upinzani lililo uhamishoni la Ginbot 7 si makundi ya kigaidi.
Mwezi uliopita pia, Ethiopia na Eritrea zilikubaliana kurejesha tena uhusiano wao kidiplomasia na kufungua ofisi za kibalozi katika miji mikuu ya nchi hizo, baada ya majirani hao kuhasimiana kwa karibu miongo miwili na wengi wanalitaja hilo kama juhudi za Abiy Ahmed za kuleta mageuzi ya kisiasa na kiuchumi.