Wanaharakati Misri wataka kuachiwa huru wapinzani
(last modified Tue, 28 Aug 2018 09:05:59 GMT )
Aug 28, 2018 09:05 UTC
  • Wanaharakati Misri wataka kuachiwa huru wapinzani

Muungano wa wanaharakati wa kisekulari na mrengo wa kushoto nchini Misri umekemea hatua ya vyombo vya usalama nchini humo ya kuwatia nguvuni shakhsia kadhaa wa upinzani na kutoa wito wa kuachiwa huru wafungwa wote wasiokabiliwa na tuhuma za kuhusika na machafuko.

Balozi wa zamani wa Misri, Masoum Marzouk na wanaharakati wengine sita walitiwa nguvuni Alkhamisi iliyopita na watashikiliwa jela kwa kipindi cha siku 15 kwa uchunguzi wa tuhuma za kujiunga na makundi ya kigaidi na kupokea fedha kutoka kwa makundi hayo.

Siku chache zilizopita Balozi Masoum Marzouk alitoa wito wa kufanyika kura ya maoni kuhusu uongozi wa Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri, hatua ambayo imetajwa kuwa ni ya aina yake ya kukosoa utawala wa Jenerali huyo mstaafu.

Taarifa iliyotolewa na kundi hilo linalojulikana kwa jina la The Civil Democratic Movement (CDM) imepinga mbinu za kipolisi zinazotumiwa kukabiliana na wapinzani.

Wapinzani wengi wa al Sisi wameswekwa jela.

Imesema mbinu hizo ni sehemu ya sera zinazotumiwa na utawala wa sasa wa Cairo kunyamazisha sauti yoyote inayopinga sera za kidhalima zinazokandamiza demokrasia.

Katika miaka ya hivi karibuni serikali ya Misri imewatia nguvuni na kuwafunga jela maelfu ya wapinzani wake, wengi wao wakiwa ni wanaharakati wa Kiislamu.

Tags