Bosco Ntangada wa DRC akiwa ICC: Mimi si mhalifu ni mwanamapinduzi
Mbabe wa zamani wa kivita wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Bosco Ntanganda, amedai mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, kuwa yeye si mhalifu bali ni mwanamapinduzi.
"Ntaganda anakabiliwa na mashtaka ya kuwapa madawa ya kulevya na pombe askari watoto kabla ya kuwatuma kuua maadui zake huko Ituri, mashariki mwa DRC," wawakilishi wa waathirika wa mambo hayo wamesema mbele ya ICC katika mashtaka yao dhidi ya mbabe huyo wa kivita.
Jumanne wiki hii upande wa mashtaka ulionyesha orodha ya visa vya mauaji yaliyofanywa chini ya amri ya Ntaganda katika kipindi cha kuanzia mwaka 2002 hadi 2003 katika kaskazini mwa DRC wakati wa ufunguzi wa awamu ya mwisho ya kesi yake kewnye mahakama ya ICC.
Ntaganda ambaye anafahamika kwa jina maarufu la "The Terminator" anakabiliwa na makosa 13 ya uhalifu wa kivita na matano ya uhalifu dhidi ya ubinadamu katika eneo la Ituri la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambayo mwezi Septemba 2015 alikana kuyatenda. Anashutumiwa kuwa ameamuru mauaji, uporaji na ubakaji uliofanywa na askari wake. Katika kikao cha Alkhamisi cha ICC, mawakili wa Ntaganda walidai kwamba alikuwa akiwalinda watoto wa wanajeshi waliokuwa chini ya usimamizi wake.

Maazimio ya mwisho yalifunguliwa Jumanne wiki hii karibu miaka mitatu baada ya kesi ya Ntaganda kuanza kusikilizwa ICC mjini Hague Uholanzi, ambako ndiko anakoshikiliwa hivi sasa mbabe huyo wa zamani wa kivita.
Iwapo atapatikana na hatia basi atafungwa miaka 30 huku baadhi ya weledi wakisema Ntaganda atafadhilisha kufungwa katika gereza lolote la nchi ya Ulaya kuliko kukamatwa na kufungwa jela Rwanda au DRC.