Wapinzani waendelea na maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi nchini Mali
-
Rais Ibrahim Boubacar Keita wa Mali
Wapinzani wa serikali ya Mali kwa mara nyingine tena wamefanya maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais.
Jeshi la polisi la Mali limetangaza kuwa, maelfu ya wapinzani wa serikali jana walifanya maandamano mjini Bamako kupinga ushindi wa Rais Ibrahim Boubacar Keita katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais.
Soumaïla Cissé, mgombea wa upinzani aliyeshindwa katika uchaguzi huo, naye alikuwemo kwenye maandamano hayo.
Kwa mujibu wa jeshi la polisi la Mali, waandamanaji walipiga mayowe ya kuilaani serikali na kulalamikia kutiwa mbaroni bila sababu wakuu wawili wa kambi ya upinzani.
Wapinzani nchini Mali wakiongozwa na Soumaïla Cissé wameuamua kufanya maandamano kila siku ya Jumamosi kupinga matokeo ya uchaguzi huo yaliyompa ushindi Rais Keita na matokeo hayo kupasishwa na Mahakama ya Katiba. Maandamano hayo ya wapinzani yalianza tarehe 20 mwezi ulioisha wa Agosti.
Duru ya pili ya uchaguzi wa rais wa Mali ilifanyika tarehe 12 Agosti na tume ya uchaguzi ikatangaza kuwa Keita ameshinda uchaguzi huo kwa asilimia 67 ya kura dhidi ya mpinzani wake, Soumaïla Cissé.
Mahakama ya Katiba ilipasisha matokeo hayo tarehe 20 Agosti na kutupilia mbali mashtaka yote yaliyofunguliwa dhidi ya ushindi huo wa Keita.